Mchango wa Lugha za Kiasili katika Uafikiaji wa Maendeleo Endelevu
Abstract
Makala hii inajadili dhima ya lugha za kiasili, ikiwemo ya Kiswahili,
katika kuafikia maendeleo endelevu barani Afrika. Kimsingi, asilimia kubwa ya
wenyeji wa bara hili huishi katika maeneo ya mashambani na huzitumia lugha za
kiasili katika mawasiliano ya kila siku. Kati ya sekta muhimu zinazoathiriwa na
matumizi ya lugha ni pamoja na elimu, habari na mawasiliano, burudani, dini,
uandishi na uchapishaji, utunzaji na uhifadhi wa mazingira, afya, kilimo na
biashara. Aidha, upatikanaji wa maendeleo endelevu utategemea kwa kiasi
kikubwa iwapo wananchi watashirikishwa katika aina mbalimbali za utafiti na
matokeo yake kuwasilishwa kwa lugha wanayoielewa ili waweze kuyatekeleza.
Makala hii inachukulia kuwa lugha inayo dhima kuu katika utekelezaji wa huduma
na shughuli mbalimbali za kitaaluma.