Umbuji wa Wahusika katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano Kutoka kwa Diwani ya Jicho la Ndani (S.A. Mohamed, 2002).
Abstract
Suala la utunzi na uhakiki wa mashairi ya Kiswahili limejadiliwa kwa muda mrefu na washairi na wataalamu
mbalimbali. Mjadala huu umejikita katika dhana na maana ya shairi la Kiswahili na iwapo lihakikiwe kwa kuzingatia
kaida zilizowekwa na wanamapokeo au uhuru ulioibuliwa na wanamapinduzi. Hali hii imekinza kwa kiasi fulani
uzingatiaji kikamilifu wa mbinu nyinginezo za kiubunifu za kulihakiki shairi la Kiswahili. Kati ya vipengele muhimu
katika sanaa hii kongwe vilivyotelekezwa kiasi ni uteuzi wa wahusika, uchunguzi wa mazingira wanamopatikana na hisia
wanazotumiwa na mshairi kuwasilisha, kama inavyosisitizwa katika Nadharia ya Ulimbwende. Kimsingi, jamii
husawiriwa katika kazi za fasihi kupitia wahusika kwani ndio wawakilishi na viwakilishi vya hali halisi za wanajamii.
Jinsi mshairi akatavyowateua na kuwasawiri wahusika wake katika mazingira mahsusi itaifanya hadhira kuyapenda au
kuyachukia matendo, tabia na hali fulani za wanajamii waliowakilishwa na wahusika hao. Makala haya yananuiwa
kubainisha dhima ya wahusika wa kishairi katika kujadili na kuhifadhi masuala ya kihistoria.